MAHAKAMA YA MAPENZI
Friday, February 12, 2016
NEY AWAKEJELI BASATA
LICHA ya kufungiwa kwa wimbo wa msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Nay wa Mitego uitwao Shika adabu yako, msanii huyo ameonekana kutojutia uamuzi huo uliotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Juzi Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza alitoa tamko la kuufungia wimbo huo kutokana na kubeba ujumbe ambao unakejeli na kudhalilisha baadhi ya wasanii.
Pia katika hoja zake za kuufungia wimbo huo Mngereza alisema kuwa msanii huyo amejidhalilisha mwenyewe pia kwa kuwa ameshindwa kufuata misingi na maadili ya kazi yake.
Akizungumza kuhusiana na kufungiwa kwa wimbo huo msanii huyo ambaye katika wimbo wake huo pia amekejeli utendaji wa baraza hilo, alisema kuwa baraza hilo limechelewa kuufungia wimbo wake kwani tayari kila mtu anao.
Alisema kuwa wapo wasanii ambao amegusia maisha yao na kuonekana kuwa ni kama vile ameingilia maisha ya watu binafsi ila kwa upande wake amefanya kazi yake kama msanii.
“Najua nikisema kuwa Ray mtu mzima na amekuwa anafanya sanaa ya filamu muda mrefu lakini anaishi kwao, hapo nimekosea nini mimi naona ni kama vile nimefundisha kwanza,” alisema msanii huyo.
Alisema: “Wasanii wamekuwa wakipenda kuwasema watu wengine na wao hawasemwi na hapo tunakuwa hatujajifunza kabisa na mimi nimewakumbusha kitu”.
Wasanii waliotajwa kwenye wimbo huo ni Wema Sepetu, Ray na wengine wengi huku akilisema Basata kuwa ni baraza lisiloweza kung’ata.
Nay wa Mitego amekuwa kwa muda mrefu akilaumiwa kwa nyimbo zake ambazo zimeonekana kuwakejeli watu wa aina mbalimbali na kwa miaka mingi amekuwa akifanya hivyo.
Aliwahi kuimba wimbo uitwao Nasema Nao ambao nao ulikuwa ukigusia maisha binafsi ya wasanii wa aina mbalimbali wa muziki wa Bongo Fleva na Filamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment